Cruz mbele ya Trump utafiti wa maoni Iowa

Ted Cruz Haki miliki ya picha EPA
Image caption Ted Cruz amekuwa akiwavutia sana Wakristo wahafidhina wa Iowa

Utafiti wa maoni uliofanywa miongoni mwa wafuasi wa chama cha Republican jimbo muhimu la Iowa umemuonyesha Seneta wa Texas Ted Cruz akiwa mbele ya Donald Trump, ambaye anaongoza kitaifa.

Utafiti huo wa maoni, uliofanywa na magazeti ya Bloomberg Politics na The Des Moines Register, umeonyesha Bw Cruz akiwa na asilimia 10 mbele ya Bw Trump.

Iowa husaidia kutoa mwelekeo kwa kinyang’anyiro cha kuteua wagombea wa urais Marekani kwani huwa jimbo la kwanza kuandaa kongamano la kuteua wagombea.

Kura hiyo ya hivi karibuni zaidi inaonyesha huenda kukawa na kinyang’anyiro kikali cha kuteua mgombea wa chama cha Republican.

Kwa mujibu wa jarida la New York Times, Bw Cruz huenda akaishia kupendwa zaidi na wafuasi wa Republican wanaoegemea siasa za mbali kulia badala ya Bw Trump.

Bw Cruz na Bw Trump wamekuwa wakifanya kampeni kali Iowa, na wanatumai ushindi Februari 1 utatia nguvu azma yao ya kuwania tiketi ya kusaka urais.

Kwenye utafiti huo wa maoni, 31% ya waliohojiwa walitaka Bw Cruz ateuliwe mgombea, wakilinganishwa na 21% wa Bw Trump.

Bw Trump alikuwa ameshambulia The Des Moines kabla ya matokeo ya utafiti huo kutolewa, akisema gazeti hilo si la kuaminika.

Bw Trump na Bw Cruz pia wamekuwa wakijibizana kupitia taarifa na pia kwenye Twitter, na kuibua hisia kwamba huenda mkataba usio rasmi kati ya wawili hao umetibuka.

Awali, walionekana kuwa marafiki.

Haki miliki ya picha Getty
Image caption Trump bado anaongoza kwenye kura za maoni kitaifa

Kura ya maoni ya kitaifa iliyofanywa na NBC News/Wall Street Journal pia imeonyesha Bw Cruz akipanda hadi nambari mbili nyuma ya Bw Trump, huku Ben Carson akishuka asilimia 18 hadi nambari nne.

Bw Trump anasalia kuwa maarufu zaidi kitaifa, kwa mujibu wa kura nyingi za maoni.