Uturuki yaanza kuondoa majeshi Iraq

Iraq Haki miliki ya picha Getty
Image caption Iraq ilipinga vikali hatua ya Uturuki kutuma wanajeshi 150

Uturuki imesema inaondoa baadhi ya wanajeshi wake waliokuwa wameingia Iraq, kwa mujibu wa shirika la habari la serikali.

Shirika hilo la Anadolu limewanukuu maafisa wa jeshi wakisema msafara wa kati ya magari 10-12 ya kijeshi umeondoka kambi ya Bashiqa na kuelekea kaskazini.

Uturuki ilituma wanajeshi wake katika eneo hilo lililo karibu na jiji la Mosul, linalodhibitiwa na wapiganaji wanaojiita Islamic State, tangu 2014 kutoa mafunzo kwa wapiganaji wa Kikurdi nchini Iraq.

Lakini hatua yake ya kutuma wanajeshi 150 zaidi mwezi huu ilipingwa vikali na serikali ya Iraq.

Baghdad ilisema hatua hiyo ilichukuliwa bila mashauriano na kwamba ilikiuka uhuru na mipaka ya Iraq na pia kuvunja sheria za kimataifa.

Iraq ilikuwa imetoa wito kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuishurutisha Uturuki kuondoa wanajeshi hao.

Ankara ilijitetea na kusema wanajeshi walioingia Iraq walikuwa sehemu ya wanajeshi wa kawaida wanaotumwa huko chini ya ujumbe wa kimataifa wa kutoa mafunzo kwa wapiganaji wa Iraq wanaokabiliana na Islamic State (IS).

Lakini Ijumaa, Waziri Mkuu wa Uturuki Ahmed Davutoglu alisema taifa lake limeamua kupanga upya wanajeshi wake Bashiqa kufuatia mazungumzo na maafisa wa Iraq.