Obama: Tumeipiga IS kwa nguvu Novemba

Haki miliki ya picha EPA
Image caption Rais wa Marekani ametathimini Operesheni dhidi ya ISIL

Rais wa Marekani, Barack Obama amesema vikosi vya Marekani vinawashambulia wanamgambo wa Islamic State kwa nguvu kuliko wakati mwingine.

Akiongea katika mkutano na waandishi wa habari katika wizara ya ulinzi nchini humo, Obama amesema mashambulizi zaidi ya anga yametekelezwa dhidi ya kundi hilo mwezi Novemba kuliko mwezi mwingine wowote.

Muungano wa ndege za mashambulizi ya anga, wapiganaji, ndege za mashambulizi ya mabomu na ndege zisizo na rubani vimeongeza kasi ya mashambulizi ya anga na kufikia 9,000 mpaka sasa.

''Mwezi uliopita wa Novemba, tuliangusha mabomu zaidi kwenye maeneo ya ISIL kuliko mwezi mwingine wowote tangu kampeni hii ilipoanza, pia tunawaua viongozi wa IS, makamanda wao na wauaji mmoja baada ya mwingine," amesema Obama.

Hata hivyo amekiri, kuwa kutokana na mashambulizi ya kigaidi ya hivi karibuni, jitihada zaidi zinahitajika.

''Tunatambua kuwa jitihada zinahitajika haraka. Hakuna anayejua raia wangapi wa Syria na Iraq wanaoathirika kutokana na vitendo vya kigaidi vya IS pia na familia za San Bernardino na Paris na kwingine ambako wanaomboleza vifo vya wapendwa wao,'' amesema Rais Obama.