Katanga na Lubanga kufungwa jela DR Congo

Katanga Haki miliki ya picha ICC
Image caption Bw Germain Katanga

Viongozi wa zamani wa waasi Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo Thomas Lubanga na Germain Katanga wamepelekwa DR Congo wakakamilishie vifungo vyao huko.

Wawili hao walifungwa jela na Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu wa Kivita (ICC) baada ya kupatikana na makosa ya uhalifu wa kivita.

Hii ni mara ya kwanza kwa ICC kuwatuma wafungwa nje wakatumikie vifungo vyao.

Afisi ya Rais wa mahakama ya ICC ilitangaza DR Congo kuwa taifa litakalotumiwa kutekeleza vifungo vya wawili hao Desemba 8.

Image caption Bw Thomas Lubanga

Afisi hiyo ilisema Thomas Lubanga Dyilo na Germain Katanga wenyewe walikuwa wameeleza mapenzi ya kwenda kutumikia vifungo vyao taifa lao la kuzaliwa.

Mahakama ya ICC itaendelea kufuatilia kufungwa kwao kuhakikisha wanawekwa katika “mazingira yafaayo kimataifa ya kuwazuilia wafungwa”.

Wawili hao wamehamishiwa DR Congo kupitia ushirikiano wa karibu kati ya maafisa wa DR Congo, Uholanzi na Ufaransa.

Lubanga alihukumiwa kifungo cha miaka 14 jela tarehe 10 Julai, 2012 baada ya kupatikana na makosa ya kuwaandikisha watoto kwenye jeshi na kuwatumia vitani.

Mahakama ya rufaa ilidumisha hukumu hiyo Desemba 2014. Lubanga amekuwa kizuizini The Hague tangu 16 Machi 2006 na ukizingatia muda aliokaa kizuizini kabla ya kuhukumiwa, basi huenda akaachiliwa huru kabla ya 2020.

Katanga alihukumiwa kifungo cha miaka 12 jela kwa maoksa ya kushiriki kosa la uhalifu dhidi ya binadamu na makosa manne ya uhalifu wa kivita ya kuua, kushambulia raia na kuharibu mali kijiji cha Bogoro, Ituri mashariki mwa Dr Congo.

Anatarajiwa kukamilisha kifungo chake tarehe 18 Januari 2016.