Bomu lapatikana kanisani Kenya

Image caption Bomu lapatikana kanisani Kenya

Waumini katika kanisa moja nchini Kenya wanakila sababu ya kumshukuru mola wao baada ya bomu iliyokuwa imetegwa ndani ya kanisa kupatikana wakati wa ibada.

Waumini hao wa kanisa katoliki la Kutus lililoko eneo la katikati ya nchi walitoroka kanisani baada ya muumini mmoja kuona kifaa kilichokuwa kimefichwa chini ya viti alipokuwa akitoa sadaka na kuwatahadharisha wenzake.

''Tulipokuwa tukienda kutoa sadaka niliona kitu kilichokuwa kinafanana kama kisanduku kidogo na nyaya ,nilihofu sana nikamweleza padri'' alisema bwana Richard Kanyuiro.

Afisa mmoja wa polisi wa utawala aliyeitwa kushuhudia alikitambua kifaa hicho kuwa ni bomu na hivyo wakawaarifu waumi waliotorokea usalama wao.

Maafisa wa usalama kutoka Nyeri na Embu waliitwa na kuwaondoa waumi wote karibu na kanisa hilo huku wakiwasubiri maafisa wenye uwezo wa kuharibu mabomu kuwasili kutoka Nairobi.

Mwenyekiti wa waumini katika eneo hilo bwana Paul Njeru, anasema kuwa huenda kilipuzi hicho kiliwekwa mapema siku ya jumapili katika sala ya alfajiri kwa nia ya kukilipua wakati wa misaa.

Kasisi Njenga anayesimamia kanisa hilo anasema ilikuwa ni bahati tu na huruma ya mwenyezi mungu kuwa kifaa hicho hakikulipuka wakati waumini wamejaa kanisani.

''Ni mkono wa mungu tu kuwa kilipuzi hichi hakikulipuka wakati wa ibada''

Majuzi tu Idara ya polisi nchini Kenya ilitangaza tahadhari mbali na kutaja majina ya washukiwa 11 wa ugaidi wanaodaiwa kuwa wameingia humu nchini kutoka somalia kwa nia ya kutekeleza mashambulizi haswa wakati huu wa krismasi.