Air France: Abiria 2 wakamatwa Paris

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Abiria 2 wakamatwa Paris

Maafisa wa polisi nchini Ufaransa wamewatia mbaroni mume na mkewe waliokuwa abiria katika ndege ya Air France iliyolazimika kutua kwa dharura nchini Kenya hapo jana kufuatia tishio la bomu ikiwa angani.

Duru zinasema kuwa wawili hao ambao majina yao bado hayajatangazwa hadharani walikamatwa punde baada ya kutua katika uwanja wa kimataifa wa Charles de Gaulle.

Haki miliki ya picha r
Image caption Ndege hiyo ilikuwa na abiria 459 na wahudumu 14.

Frederic Gagey aliwaambia waandishi wa habari mjini Paris Ufaransa kuwa kifaa kilichodhaniwa kuwa kilipuzi kilikuwa ni mbao na kisanduku cha karatasi tu wala hakikuwa na uwezo wowote wa kuhatarisha usalama wa ndege hiyo.

Ndege hiyo ya Ufaransa chapa Boeing 777 nambari AF463 inayohudumu kati ya Mauritius na Paris ililazimika kutua baada ya kile kinachotajwa kuwa bomu bandia.

Inasemekana kuwa abiria mmoja alikipata kifaa hicho chooni na akamfahamisha mhudumu mmoja wa ndege hiyo.

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Mume na mkewe wamekamatwa walipotua mjini Paris

Mhudumu huyo alimfahamisha rubani kuhusiana na kifaa hicho na shughuli za kutua kwa dharura zikaanza.

Ndege hiyo ilitua saa sita usiku wa kuamkia Jumapili, huku wataalamu wa kutegua mabomu kutoka jeshi la wanamaji la Kenya wakiingia ndani ya ndege hiyo kukagua kifurushi kilicholeta taharuki.

Sasa kitengo cha ujasusi cha Ufaransa kimeanzisha uchunguzi wa kina kubaini kilichosababisha tishio hilo.