Uharamia bado tishio Somalia

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Meli za uvuvi nchini Somalia

Mkuu wa Operesheni dhidi ya uharamia katika eneo la Bahari ya Hindi Meja Jenerali Martin Smith ametahadharisha kwamba maharamia kutoka Somalia bado ni tishio na kwamba kimya chao kwa sasa ni kutokana na kukosa fursa ya kufanya uvamizi.

Amesisitiza kuwa mtandao huo kwa sasa unakwamishwa na uwepo wa vikosi vya kimataifa ambavyo vimekuwa vikiendesha doria ndani ya Bahari ya Hindi.

Eneo la Bahari ya hindi nchini Somalia fukwe zake zilitajwa wakati mmoja kuwa ni hatari zaidi duniani, kutokana na matukio ya utekaji wa meli unaotekelezwa na maharamia kutoka nchini humo. Mwezi uliopita Meli za uvuvi za Iran na Thailand zilivamiwa pwani ya Somalia japo kuwa kwa sasa kuna hali ya utulivu dhidi ya uvamizi huo.

Jumuiya za kimataifa ziliingilia kati hali hiyo kwa kuleta vikosi vya kufanya doria katika eneo hilo, ambapo majeshi ya NATO,Jumuiya ya Ulaya EU,na muungano wa majeshi ya Marekani kwa sasa wamedhibiti eneo hilo.

Hali hii ya utulivu na kukosekana kwa matukio ya utekaji kwa sasa katika eneo hilo inaelezwa kuwa imetokana na harakati za kiusalama zinazoendeshwa na vikosi hivyo vya kimataifa, hali inayosababisha meli za kigeni kuja katika anaeo hilo kwaajili ya uvuvi na hivyo kuwanyima fursa wavuvi wa Somalia.

Meja Jenerali Smith kutoka Muungano wa vikosi vya majini kutoka Jumuiya ya Ulaya, anasema kuwa utulivu huo wa utekaji ni wa muda tu, na ni matokeo ya jitihada za vikosi hivyo ,ambapo ameisisitiza serikali ya Somalia kuwa na mikakati ya muda mrefu kuhakikisha wanaimarisha hali ya ulinzi na usalama katika mwambao huo wa Bahari ya Hindi nchini humo.

Kwa sasa nchi ya Somalia pamoja na kuwa na eneo pana zaidi barani Afrika kwa shughuli za uvuvi lakini bado nchini humo hakuna sera madhubuti za kulinda maeneo hayo na pia hakuna mikakati ya kudumu na endelevu.