Nigeria: Buhari asoma makadirio ya bajeti

Haki miliki ya picha AP
Image caption Buhari asoma makadirio ya Bajeti

Rais wa Nigeria Muhammadu Buhari amewasilisha makadirio ya bajeti ya kwanza tangu kuchaguliwa kwake, katika wakati ambapo bei ya mafuta duniani imepungua kwa kiwango kikubwa.

Mafuta ni bidhaa muhimu zaidi nchini Nigeria inayouzwa kwa mataifa ya nje.

Rais Buhari anasema serikali yake imepanga kutumia takriban dola bilioni 31 mwaka ujao, ambalo ni ongezeko la asilimia 20, katika maendeleo ya miundo mbinu na ushindani.

Uchumi wa taifa hilo umekuwa ukikwazwa na ufisadi, ambao rais Buhari ameahidi kuangamiza.

Kusomwa kwa bajeti kumefanyika siku 10 kabla ya mwisho wa mwaka.

Haki miliki ya picha
Image caption Bajeti hiyo imeongezwa kwa asili mia 20% ikilinganishwa na ile ya mwaka jana, chini ya serikali ya awali.

Bajeti hiyo imeongezwa kwa asili mia 20% ikilinganishwa na ile ya mwaka jana, chini ya serikali ya awali.

Rais Muhammadu Buhari alisema bajeti hiyo itashughulikia ukosefu wa ajira hasa miongoni mwa vijana mbali na kuimarisha maisha ya wa-NIgeria maskini.

Alisema atatoa malipo kwa wa-Nigeria walalal hoi kupita mpango maalum alioutaja kama wa kutoa pesa taslimu, na pia kutekeleza mpango wa chakula kwa shule kwa watoto katika shule za umma.

Lakini hakusema ni kiasi gani cha pesa atawalipa maskini na ni wangapi watalipwa.

Pia haijabainika wazi jinsi serikali inavyowatambua maskini.

Kwa kutoa matumaini ya kuboresha maisha kwa wa-Nigeria, makadirio ya matumizi ya serikali yalibashiriwa kulingana na bei ya mafuta ya dola 38 kwa pipa, na uzalishaji wa mafuta wa pipa bilioni 2.2 kila siku.

Haki miliki ya picha Getty
Image caption Nigeria inategemea uuzaji wa mafuta kwa asili mia 70% kwa mapato yake ya kigeni.

Lakini bei ya mafuta ilishuka hadi dola 36 kwa pipa hapo jana.

Nigeria inategemea uuzaji wa mafuta kwa asili mia 70% kwa mapato yake ya kigeni.

Rais Buhari alisema serikali yake inalenga kuziba mapungufu ya kifedha ya bajeti hiyo kwa kuongeza ushuru kwa bidhaa zisizokuwa za mafuta na kuomba mikopo.

Takribani dola bilioni mbili imetengewa sekta ya elimu, afya ikapata dola bilioni 1.2, ilhali idara ya ulinzi, ambayo mwaka jana ilitengewa pesa nyingi, itapata kiasi kidogo cha dola bilioni moja.