Saudi Arabia yabatilisha hukumu ya kifo

Image caption Saudi Arabia yabatilisha hukumu ya kifo

Sri Lanka inasema kuwa Saudi Arabia imefutilia mbali amri ya kuuawa kwa mwanamke mmoja kutoka Sri Lanka kwa kumpiga mawe.

Mwanamke huyo alikuwa amehukumiwa kwa kosa la kuzini.

Alikuwa akifanya kazi za nyumbani nchini Saudia.

Hukumu ya mwanamke huyo aliye na watoto wawili ilizua maandamano makali nchini Sri lanka.

Serikali ya Sri lanka ilikaribisha hatua ya Saudi Arabia ya kusikizwa upya kesi ya mwanamke huyo.

Sasa Saudi Arabia inasema mwanamke huyo hatouawa kwa kupigwa kwa mawe, hukumu inayokabidhiwa washukiwa wa uzinzi, chini ya sheria kali za kiislamu zinazofuatwa na taifa hilo.

Mwaka huu kumekuwa na lalama za kimataifa kuhusu mfumo wa haki nchini Saudi Arabia, na inaonekana zimekuwa na matokeo.

Kupigwa mijeledi kwa mwanablogu aliyezuliwa gerezani, Raif Badawi, kulisitishwa baada ya shinikizo kutoka kote duniani, huku mwanamme mmoja kutoka Uingereza akirejeshwa nyumbani badala ya kupigwa mijeledi, baada ya kupatikana na pombe.