Serikali CAR yataka uchaguzi uahirishwe

CAR
Image caption Watu 2 milioni wamejiandikisha kupiga kura CAR

Serikali ya mpito nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati imependekeza uchaguzi mkuu nchini humo uahirishwe kwa siku tatu.

Uchaguzi wa urais na ubunge ulipangiwa kufanyika Jumapili lakini serikali inasema maandalizi hayajakamilika na inataka uahirishwe hadi Desemba 30.

Pendekezo hilo lilitolewa Alhamisi kwenye mkutano uliohudhuriwa na wawakilishi wa wagombea, vyama vya siasa, tume ya uchaguzi na jamii ya kimataifa.

“Tarehe 30 Desemba itakuwa bora kwetu,” mkuu wa tume ya uchaguzi Marie-Madeleine

N'kouet Hoornaert alisema alipoulizwa na Rais wa mpito Catherine Samba Panza kuhusu wakati mwafaka wa kufanyika kwa uchaguzi huo.

Mabadiliko yoyote kwenye siku ya uchaguzi yatahitajika kuidhinishwa na Mahakama ya Kikatiba kwani sheria ya sasa inataka uchaguzi ufanyike siku a Jumapili.

Haijabainika ni lini mahakama hiyo ingekutana kujadili hilo.

Umoja wa Mataifa umesema kuahirishwa kwa uchaguzi huo, ambao tayari umecheleweshwa, hakutaathiri pakubwa mchakato wa kuwatafuta viongozi wapya.

“Siwezi kutaja hilo kama pigo” kwa shughuli hii ya kisiasa, msemaji wa UN Stephane Dujarric amesema.

Alieleza kuwa karatasi zote za kura ziliwasili mji mkuu Bangui Jumatano na walinda Amani wa UN kwa jina MINUSCA wataendelea kufikisha karatasi hizo maeneo mbalimbali ya nchi.

Uchaguzi huo unatarajiwa kurejesha uthabiti kwenye taifa hilo lililotikiswa na machafuko tangu waasi wa Kiislamu walipompindua kiongozi Mkristo Francois Bozize mwaka 2013.

Jumatatu, maafisa wa uchaguzi walisema kura ya maamuzi iliyokuwa imeandaliwa kuidhinisha uchaguzi wa urais na ubunge ilikuwa imeungwa mkono na asilimia 93 ya wapiga kura.