Mateka wa Iran kulipwa miaka 36 baadaye

Mateka Haki miliki ya picha AP
Image caption Mateka 53 walizuiliwa kwa siku 444 ubalozi wa Marekani mjini Tehran

Wamarekani waliozuiliwa mateka nchini Iran watalipwa fidia miaka 36 baada ya kisa hicho, ripoti zinasema.

Kila mmoja kati ya mateka hao 53, au jamaa zake, atapokea fidia ya $4.4m (£3m), kwa mujibu wa mswada wa matumizi ya pesa Marekani ambao ulipitishwa Ijumaa.

Waathiriwa wa mashambulio mengine ya kigaidi yaliyofadhiliwa na dila, kama vile mashambulio ya bomu katika balozi za Marekani Afrika Mashariki mwaka 1998 pia watakuwa na nafasi ya kulipwa fidia.

Wamarekani hao walizuiliwa mateka siku 444, na kisa hicho kilipelekea Marekani kukatiza uhusiano wake na Iran.

Uamuzi wa kulipa fidia umetokea baada ya mwafaka tata uliotiwa saini kati ya mataifa yenye ushawishi mkubwa duniani na Iran kuhusu mpango wake wa nyuklia.

Matekani hao wamepigania fidia kwa miaka mingi lakini mwafaka uliofanikisha kuachiliwa kwao ulikuwa na kifungu cha kuwazuia kuwasilisha madai ya fidia.

Majaribio yao mara kwa mara yalizuiwa na mahakama, ikiwa ni pamoja na rufaa iliyokataliwa na Mahakama ya Juu.

Bunge halikuweza kupitisha sheria za kuwalipa fidia.

Pesa watakazolipwa sasa huenda zikatoka kwa faini kubwa ya $9bn iliyotozwa benki ya Paribas ya Ufaransa kwa kukiuka vikwazo vilivyowekewa Iran, Sudan na Cuba, gazeti la New York Times limeripoti.

Jumla ya $1bn zitatumiwa kufidia waathiriwa wa ugaidi na $2.8bn zitatendwa kusaidia waathiriwa wa shambulio la 9/11 na familia zao.

Sheria hiyo mpya inatoa fursa ya kulipwa $10,000 kwa kila siku ambayo mateka alizuiliwa, huku wanandoa na watoto nao wakilipwa hadi $600,000. Malipo ya kwanza yatatolewa katika kipindi cha mwaka mmoja.

Mateka 36 kati ya 53 waliozuiliwa mateka ubalozi wa Marekani mjini Tehran ulipovamiwa bado wako hai.