Modi afanya ziara ya kushtukiza Pakistan

Modi Haki miliki ya picha AFP
Image caption Modi alikutana kwa muda mfupi na Sharif mjini Paris mwezi jana

Waziri Mkuu wa India Narendra Modi amekutana na mwenzake wa Pakistan Nawaz Sharif baada yake kufanya ziara ya kushtukiza nchini humo.

Bw Modi alikuwa safarini kurejea India kutoka Afghanistan alipoamua kutua katika mji wa mashariki wa Lahore. Ziara yake imelingana na siku ya kuzaliwa ya Bw Sharif.

Bw Modi ndiye waziri mkuu wa kwanza wa India kuzuru Pakistan tangu 2004.

Wawili hao walikumbatiana baada ya Modi kuwasili katika uwanja wa kimataifa wa ndege wa Allama Iqbal, kabla ya kufululiza hadi nyumbani kwa Bw Sharif. Baada ya mkutano huo Bw Modi aliondoka na kurejea India.

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Modi alikumbatiana na Sharif baada ya kuwasili uwanja wa ndege

Hakuna taarifa yoyote rasmi iliyotolewa na pande zote mbili kuhusu mkutano huo.

Uhusiano kati ya mataifa hayo mawili jirani, yenye silaha za nyuklia, ulikuwa umedorora kwa miaka mingi lakini sasa umeanza kuimarika.

Wawili hao walikutana kwa muda mfupi mjini Paris mwezi jana pembezoni mwa mkutano kuhusu mabadiliko ya hali ya hewa duniani wa COP21.

Mataifa hayo yamepigana vita mara tatu tangu kujipatia uhuru kutoka kwa Uingereza, vita vivili kuhusu jimbo la Kashmir.

Mataifa yote mawili hudai eneo lote la Kashmir, jambo ambalo yamezozania kwa zaidi ya miaka 60 sasa.

Makubaliano ya kusitisha mapigano yalitiwa saini mwaka 2003, lakini mara kwa mara kila upande hudai mwenzake ameukiuka.