Mazungumzo ya kutafuta amani Burundi kuanza

Haki miliki ya picha
Image caption Burundi:Mazungumzo ya amani kuanza Kampala

Mazungumzo ya kusuluhisha mzozo wa Burundi yataanza tena leo mjini Kampala, chini ya usimamizi wa rais Yoweri Museveni wa Uganda.

Museveni aliteuliwa na Jumia ya Afrika Mashariki kuongoza mchakato wa amani ya Burundi, kufuatia machafuko yaliozushwa na uamuzi wa rais Pierre Nkurunziza kupigania muhula wa tatu, kinyume cha maana ya mapatano ya Arusha na katiba ya Burundi inayoruhusu mihula miwili.

Mamia ya Warundi wanasemekana kuuawa na maelfu kukimbia makwao.

Makundi 14, yakiwakilisha masilahi mbalimbali ya Warundi, yatashiriki mkutanoni.

Mwandishi wa BBC wa Kampala, Alli Mutasa, anaripoti kuwa sababu mazungumzo ya amani ya Burundi yamekawia kuanza, hadi Desemba 28, ilitokana na shida ya kuyajumuisha makundi yote husika, kwa mujibu wa Waziri wa Ulinzi wa Uganda, Crispus Kiyonga.

“Haikuwa rahisi,” alisema. Na baada ya kuzinduliwa rasmi mjini Kampala leo, mazungumzo hayo yatahamishiwa Arusha Tanzania, ila pakizuka neno.

Chama tawala CNDD-FDD na makundi kadha dhidi ya serikali ya Nkurunziza, vitahudhuria aliongeza Dk Kiyonga.

Haki miliki ya picha
Image caption Mamia ya Warundi wanasemekana kuuawa na maelfu kukimbia makwao.

Agenda ya mazungumzo haijulikani wazi.

Bila shaka amani ndio kiini cha mazungumzo haya, na vipi ipatikane.

Zaidi ya wiki moja iliopita, Muungano wa Afrika, ulipendekeza kutuma kikosi cha askari 5,000 ili kukomesha machafuko, na kuzuia Burundi isirudie vita vya wenyewe kwa wenyewe na hata wengine kugusia ‘maangamizi ya kimbari’.

Burundi inalaani mashauri hayo kama ‘uvumi’ uso ‘msingi’, na kukana machafuko yamefikia kiwango hicho.

Serikali inashikilia kuna amani nchini ila sehemu fulani-fulani za mji mkuu Bujumbura.

Hivyo serikali si tayari kukikubali kikosi cha Muungano wa Afrika, na kikipelekwa kwa kifua, kitakabiliwa kama cha ‘uvamizi’.

Haki miliki ya picha
Image caption Serikali inashikilia kuna amani nchini ila sehemu fulani-fulani za mji mkuu Bujumbura.

Tanzania, ambayo ina maelfu ya wakimbizi Warundi, pia inapinga kikosi cha Muugano wa Afrika kutumwa Burundi.

Jumane iliyopita, Waziri mpya wa Nchi za Nje wa Tanzania, Augustine Mahiga, aliunga mkono mazumngumo, sio majeshi ya kigeni, kumaliza machafuko ya Burundi.

Pia aliandama ushauriano wa kidiplomasi kuonana na makundi ya upinzani pamoja na Nkurunziza, Bujumbura, na Museveni Kampala, kwa lengo la kuyafufua mazungumzo hayo ya amani.

Umoja wa Ulaya umechangia dola laki nne unusu kuwezesha mazungumzo ya Burundi yarudiwe.

Zaidi ya watu 400 wanaripotiwa kufa katika machafuko yalioanza Aprili mwaka huu, na kama Warundi laki tatu, ni wakimbizi wa nje na ndani ya nchi.