Mbwa aliyeuawa Paris kupewa nishani ya ushujaa

Diesel
Image caption Ni wanyama 66 pekee ambao wamewahi kutunukiwa nishani hiyo

Mbwa wa polisi aliyeuawa wakati wa msako baada ya mashambulio ya Paris atatunukiwa nishani kuu ya ushujaa.

Diesel, mbwa aina ya Belgian Shepherd mwenye umri wa miaka saba, alifariki wakati wa operesheni ya kumsaka mshukiwa mkuu wa mashambulio hayo.

Mbwa huyo atatunukiwa nishani kwa jina Dickin Medal ambayo hutolewa an shirika la kuwatunza wanyama la PDSA.

Hadhi yake ni sawa na nishani ya Msalaba wa Victoria inayopewa watu mashujaa vitani.

Kitambulisha mada #JeSuisChien (Mimi ni mbwa) kilivuma sana kwenye Twitter baada ya Diesel kuuawa.

Diesel atapewa nishani hiyo kwenye sherehe mwaka ujao.

"Habari za kifo cha Diesel zilipotangazwa, watu wengi walituma jumbe za kuomboleza,” anasema mkurugenzi mkuu wa PDSA Jan McLoughlin.

"Tulipokea risala nyingi kutoka kwa watu wakitambua ushujaa wake.”

Tangu kuanza kutolewa kwa tuzo hiyo mwaka 1943, ni wanyama 66 ambao wametunukiwa kufikia sasa.

Wanyama hao ni mbwa 30 (akiwemo Diesel), njiwa wawili waliotumika kusafirisha barua wakati wa Vita Vikuu vya Pili vya Dunia, farasi watatu na paka mmoja.