Wapiganaji waondolewa Syria

Hezbollah Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Wapiganaji wa Hezbollah kutoka Lebabon wamekuwa wakisaidiana na serikali ya Syria kukabili waasi Zabadani

Wapiganaji wa makundi ya waasi Syria wameanza kuondolewa kutoka mji wa Zabadani karibu na mpaka wa Syria na Lebanon.

Wanaondolewa kupitia mkataba auliofanikishwa na Umoja wa Mataifa.

Msafara wa mabasi na ambiulensi ulifika katika mji huo Jumatatu ukitokea Lebanon kuwachukua wapiganaji pamoja na baadhi ya raia. Watasafirishwa hadi mjini Beirut, na baadaye wasafirishwe kwa ndege hadi Uturuki.

Operesheni hiyo ni sehemu ya makubaliano ya kusitisha mapigano ulioafikiwa mwezi Septemba ukiangazia mji wa Zabadani na miji mingine miwili Kaskazini.

Watu wa familia 300 kutoka miji hiyo iliyoko mkoa wa kaskazini wa Idlib pia wanahamishwa hadi uturuki, ambapo baadaye watapelekwa Lebanon.

Kamati ya Kimataifa ya Msalaba Mwekundu (ICRC) limesema maafisa wa Shirika la Msalaba Mwekundu Lebanon na Shirika la Hilali Nyekundu la Syria pamoja na Umoja wa Mataifa wanahusika katika operesheni hiyo.