Watu 20 wauawa kwenye mashambulio Nigeria

Boko Haram Haki miliki ya picha AFP
Image caption Wanajeshi wamezidisha operesheni dhidi ya Boko Haram

Watu zaidi ya 20 wamefariki kwenye mashambulio kadha yanayoshukiwa kutekelezwa na wapiganaji wa Boko Haram katika mji wa Maiduguri, nchini Nigeria.

Wengi walifariki baada ya watu kushambulia kijiji cha Dawari katika viunga vya huo Jumapili usiku.

Jeshi la Nigeria limesema lilifanikiwa kuua watu 10 walioshukiwa kuwa washambuliaji wa kujitoa mhanga.

Na mapema Jumatatu, mwanamke alijilipua watu walipokuwa wakijiandaa kuingia kwenye msikiti.

Mwandishi wa BBC aliyeko Abuja Abdullahi Kaura Abubakar anasema wengi wa wakazi wa Maiduguri, mji ulio kaskazini mashariki mwa Nigeria walikuwa wamedhani amani imerejea baada ya mashambulio kutotokea.

Lakini katika chini ya saa 24, kumetekelezwa mashambulio manne ya kujitoa mhanga, yote yakihusisha wanawake.

Mji wa Maiduguri wakati mmoja ulichukuliwa kuwa mji mkuu wa wapiganaji wa Boko Haram kundi ambalo siku za hivi karibuni limezidisha mashambulio ya kujitoa mhanga.

Sana wanatumia wanawake vijana wa umri mdogo.

Mashambulio hayo yametokea siku chache baada ya Rais wa Nigeria Muhammadu Buhari kusema majeshi yalikuwa yamewashinda wapiganaji wa Boko Haram.

Alisema wapiganaji hao hawawezi tena kutekeleza mashambulio makubwa mijini na katika kambi za jeshi.