Wanajeshi wa Iraq wafurusha IS Ramadi

Ramadi Haki miliki ya picha AFP
Image caption Operesheni ya kuukomboa mji huo ilianza Jumanne wiki iliyopita

Jeshi la Iraq limesema linadhibiti jengo kubwa la serikali ambalo lilikuwa ndio kitovu cha mapigano katika mji wa Ramadi.

Wapiganaji wa Islamic State inaonekana wameondoka katika jengo hilo.

Hata hivyo, inasemekana wametega mabomu katika maeneo kadhaa, na jeshi bado halikuwa na udhibiti wa eneo lote.

Vikosi hivyo pia vinakabiliana na upinzani katika maeneo jirani.

Haki miliki ya picha AP
Image caption Mji huo umeharibiwa sana na mapigano

Waandishi wa habari wanasema kudhibitiwa kwa mji wa Ramadi kunaonyesha ushindi mkubwa kwa serikali katika mapambano yake na wapiganaji wa IS.

Mji huo wenye Wasuni wengi umo kilomita 90 magharibi mwa Baghdad na ulitekwa na wapiganaji wa IS mwezi Mei.

Kutekwa kwa mji huo kuliaibisha sana jeshi la Iraq.

Wapiganaji wa IS wamepokonywa miji mingi waliyokuwa wameiteka nchini Iraq, huku wakiendelea kukabiliwa vikali na wanajeshi wa Iraq na wapiganaji wa Kikurdi.