Van Gaal: Sioni haja ya kujiuzulu

Gaal Haki miliki ya picha epa
Image caption Van Gaal amekabiliwa na shinikizo za kumtaka ajiuzulu

Meneja wa Manchester United Louis van Gaal, amesema haoni haja ya kujiuzulu baada ya timu yake kutoka sare ya 0-0 na Chelsea uwanjani Old Trafford.

Akizungumza baada ya mchezo kumalizika Van Gaal alisema "kama wachezaji wanaweza kucheza kwa kiwango kile wakiwa kwenye shinikizo hakuna sababu ya kujizulu".

Kocha huyo amekua kwenye shinikizo kubwa ya kumtaka kujiuzulu kufuatia kikosi hicho kuchapwa michezo minne mfululizo kipigo cha mwisho kikiwa kutoka kwa Stoke City Jumamosi walipocharazwa 2-0.

Man United wameshindwa kupata ushindi katika michezo minane ya mashindano yote waliyoshiriki msimu huu. Hii ni mara ya kwanza klabu hiyo kufanya hivyo tangu mwaka 1990.

Klabu hiyo kwa sasa imo nambari sita kwenye jedwali na alama tano nyuma ya klabu iliyo nambari nne ligini.

Haki miliki ya picha AP

Van Gaal, anaamini anaungwa mkono na wachezaji na bodi pia.

"Mzozo uliopo sasa ni mazingira ambao nyingi (wanahabari) mmechangia," alisema meneja huyo.

"Wachezaji wamejitolea kupambana. Meneja amejitolea kupigana. Wakufunzi vilevile na bodi pia ina imani na wakufunzi na meneja."

Hata hivyo, Van Gaal, anaamini kwamba anaweza kufutwa.

Haki miliki ya picha PA

"Katika ulimwengu huu wazimu wa soka, hili linaweza kufanyika siku yoyote ile na kwangu pia," alisema. "Ukizingatia kwamba ilimfanyikia Jose Mourinho, basi inaweza kunitendekea.

Mourinho alifutwa kazi na Chelsea baada ya klabu hiyo kuandikisha msururu wa matokeo mabaya, licha yake kuwaongoza kushinda taji la ligi msimu uliopita.

Meneja huyo ni mmoja wa wanaodhaniwa wanaweza kumrithi Van Gaal iwapo ataondoka Old Trafford na wakati wa mechi hiyo dhidi ya Chelsea, kunao mashabiki waliovalia mavazi yenye jina lake.