Msaidizi mkuu wa Kim Jong-un afariki

Kim Haki miliki ya picha Getty
Image caption Kim Yang-gon alihusika na uhusiano kati ya Korea Kaskazini na Kusini

Msaidizi mkuu wa kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong-un amefariki katika ajali ya barabarani, shirika la habari la serikali la KCNA amesema.

Kim Yang-gon, 73, alikuwa katibu wa chama tawala cha Wafanyakazi na alisimamia uhusiano na Korea Kusini.

Alikuwa kwenye ujumbe wa ngazi za juu kutoka Korea Kaskazini uliosaidia kupunguza uhasama kati ya Pyongyang na Korea Kusini mwezi Agosti, baada ya majeshi ya nchi hizo mbili kufyatuliana makombora.

Shirika la habari la KCNA lilimweleza kama rafiki mkuu wa Kim Jogn-un na mshirika mkuu wa mapinduzi.

Image caption Kim Yang-gon alikuwa katibu wa chama tawala

"Rafiki Kim Yang-gon, katibu wa Chama cha Wafanyakazi na mwanachama wa kamati kuu ya Politbureau... alifariki katika ajali ya barabarani saa thenashara na robo asubuhi, Jumanne, akiwa na umri wa miaka 73," KCNA ilisema, bila kutoa habari zaidi.

Shirika hilo limeongeza kuwa Kim Jong-un atahudhuria mazishi ya kiongozi huyo pamoja na maafisa 80 wakuu wa serikali.