Wadukuzi watatiza tovuti za BBC

BBC
Image caption Wasomaji walikuwa wakipokea ujumbe kwamba kurasa hazipatikani

Tovuti zote za BBC leo zimekumbwa na matatizo kwa saa kadha baada ya kuvamiwa na wadukuzi.

Matatizo yalianza mwendo wa saa 0700 GMT (saa nne mchana saa za Afrika Mashariki) na wasomaji walikuwa wakipokea ujumbe wa kuwepo kwa matatizo katika kurasa kila walipofungua habari.

Duru za BBC zinasema tatizo hilo lilisababishwa na uvamizi ambao hujulikana kwa Kiingereza kama "distributed denial of service".

Uvamizi huu hufanya ionekane kana kwamba watu wengi sana wanatembelea tovuti kiasi kwamba tovuti hulemewa na kutatizika.

Awali BBC ilisema tatizo lilitokana na “tatizo la kiufundi” . Baadaye ilitoa taarifa kutangaza kwamba huduma za kawaida zilikuwa zimerejea.

Uvamizi huo uliathiri tovuti kuu ya BBC ya Kiingereza, pamoja na tovuti nyingine ikiwemo hii ya bbcswahili.com. Huduma za iPlayer na iPlayer Radio pia ziliathirika.

Tovuti za BBC zimewahi kukumbuwa na matatizo awali. Julai 2014, huduma ya iPlayes na tovuti husika hazikuwa zinafanya kazi kwa karibu wikendi nzima.

Baadaye ilibainika kwamba tatizo lilitokana na kasoro kwenye hifadhi data ambayo hutumiwa na huduma hiyo.