Guterres akosoa EU kwa ‘kutowafaa’ wakimbizi

Guterres
Image caption Guterres anaondoka UNHCR baada ya kuongoza kwa miaka kumi

Mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia wakimbizi amekosoa juhudi za bara Ulaya katika kushughulikia wahamiaji.

Bw Antonio Guterres, ambaye anaondoka UNHCR baada ya kuongoza kwa miaka 10, ameambia BBC kwamba Muungano wa Ulaya haukuwa umejiandaa vyema kupokea wakimbizi kutoka Syria walipoanza kuwasili.

Ameongeza kuwa hata sasa muungano huo bado haujajiandaa vyema.

Amesema migawanyiko miongoni mwa mataifa ya bara hilo ilifanya juhudi za kushughulikia wakimbizi kutoratibiwa vyema, na baadhi ya wanachama wa EU walijizatiti kuzuia wakimbizi kuingia nchi zao.

Bw Guterres amesema kwa sasa kuna wahamiaji 60 milioni kote duniani ikilinganishwa na wakimbizi 38 milioni waliokuwepo mwaka 2005.

Alisema mpango wa mataifa kuchangia kwa hiari wakati wa migogoro ya kibinadamu hautoshi na kunatakiwa mpango wa haki ambao kila taifa litatakiwa kuchangia.

Hayo yakijiri, Chansela wa Ujerumani Angela Merkel, anatarajiwa kutumia hotuba yake ya Mwaka Mpya kuhimiza Wajerumani kuchukulia wakimbizi wanaoindia humo kama “fursa itakayowafaa siku za usoni”.

Kwenye hotuba hiyo atakayoitoa Alhamisi Jioni, anatarajiwa kukiri kwamba juhudi za kuwasaidia wakimbizi kutulia itagharimu muda, nguvu na pesa.

Haki miliki ya picha Reuters

Hata hivyo, atasisitiza kwamba mataifa yamekuwa yakifaidika sana kutokana na wahamiaji.

Ujerumani imewapokea zaidi ya wahamiaji 1 milioni mwaka huu, nusu yao kutoka Syria.