Watu wawili wauawa na mshambuliaji Tel Aviv

Polisi Haki miliki ya picha AFP
Image caption Polisi wanamsaka mwanamume aliyetekeleza uvamizi huo

Watu wawili wamefariki na wengine watano kujeruhiwa baada ya mtu mwenye silaha kufyatulia watu risasi kwenye baa moja Tel Aviv, polisi wa Israel wamesema.

Kisa hicho kilitokea kwenye baa iliyoko barabara ya Dizengoff katikati mwa mji huo mkuu wa Israel.

Haijabainika wazi kilichosababisha uvamizi huo, lakini kumeripotiwa msururu wa mashambulio dhidi ya Waisraeli yaliyotekelezwa na Wapalestina.

Kulingana na jarida la Jerusalem Post, Meya wa Tel Aviv Ron Huldai amewaambia waandishi wa habari waliofika eneo la tukio kuwa huenda tukio hilo lilikuwa la kigaidi lililochochewa na utaifa.

Mtu aliyeshuhudia kisa hicho ameiambia runinga ya Israeli TV kuwa mshambuliaji alikuwa mtu mwenye umri mdogo na alikuwa na bunduki ya rashasha.

Tangu 23 Desemba, takriban raia 21 wa Israel wameuwawa, wengi wao wakidungwa visu au kufyatuliwa risasi na Wapalestina.

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Visa vya Waisraeli kushambuliwa vimeongezeka karibuni

Wapalestina takriban 131 pia wameuawa. Zaidi ya nusu ya waliouwawa wanadaiwa na Israel kuwa washambuliaji.

Wengine waliuawa kwenye mapigano na wanajeshi wa Israel.

Bw Rosenfeld amesema kupitia mtandao wa Twitter kuwa uchunguzi wa kubaini iwapo uvamizi huo ulikuwa ni wa kigaidi au uhalifu umeanzishwa.