Waislamu waliogoma wafutwa kazi Marekani

Kiwanda Haki miliki ya picha Getty
Image caption Kiwanda cha Cargill huajiri wafanyakazi zaidi ya 2,100 Colorado

Waislamu 200 wanaofanya kazi katika kiwanda kimoja cha nyama Colorado, Marekani wamefutwa kazi baada yao kugoma.

Walikuwa wamegoma kulalamikia kunyimwa uhuru wa kuswali wakiwa kazini.

Wengi wao ni wahamiaji kutoka Somalia.

Msemaji wa Baraza la Uhusiano wa Wamarekani na Waislamu Jaylani Hussein anasema wafanyakazi hao katika kiwanda cha Cargill Meat Solutions walikuwa kwa muda mrefu wameruhusiwa kuswali.

Msemaji wa kiwanda hicho cha Cargill alisema kuna uhuru wa kuabudu kiwandani lakini lazima mahitaji ya kuabudu yaambatane na mahitaji ya kazi kiwandani.

Mkurugenzi mkuu wa Tume ya Haki za Kibinadamu Somalia Omar Jamal, amesema mameneja wanafaa kufahamu kwamba Waislamu huhitajika kuswali mara kadha kwa siku, hili likitegemea kipindi cha mwaka.