Putin asema Nato ni hatari kwa usalama

Putin Haki miliki ya picha bbc
Image caption Uhusiano kati ya Urusi na nchi za Magharibi uliathiriwa na mzozo Ukraine

Rais wa Urusi Vladimir Putin ametia saini karatasi mpya ya sera ya kitaifa kuhusu usalama ambayo inataja mpango wa upanuzi wa shirika la kujihami la Nato kama hatari kwa usalama.

Stakabadhi hiyo inasema “sera huru ya nyumbani na kigeni” ya Urusi imeifanya Marekani na washirika wake kuchukua hatua.

Inayatuhumu mataifa hayo kwa kujaribu kudhibiti masuala muhimu duniani.

Mzozo nchini Ukraine, ulioanza 2014, umeathiri sana uhusiano kati ya Urusi na nchi za Magharibi.

Waraka huo kwa jina Mkakati wa Usalama wa Kitaifa ulitiwa saini na Rais Putin Alhamisi, na ni wa karibuni zaidi katika msururu wa stakabadhi za serikali zinazokosoa shirika la kujihami la nchi za Magharibi la Nato.

Mwaka 2014, Urusi ilitangaza kwamba ingebadilisha sera yake ya kijeshi kuzingatia mzozo wa Ukraine na kuwepo kwa Nato mashariki mwa Ulaya.

Mshauri wa Kremlin Mikhail Popov alisema wakati huo kwamba upanuzi wa Nato miaka ya karibuni umefanya muungano huo kukaribia mipaka ya Urusi na ni hatari kwa Urusi.

Albania na Croatia zilijiunga na Nato mwaka 2009. Mwaka 2011, muungano huo ulitambua mataifa manne yaliyotaka kujiunga nao. Mataifa hayo ni Bosnia, Georgia, Macedonia, and Montenegro.

Karatasi hiyo mpya ya Urusi inasema kuongezwa kwa majeshi ya Nato karibu na mipaka ya Urusi ni “ukiukaji wa sheria za kimataifa”.

Mwandishi wa BBC wa masuala ya kidiplomasia Bridget Kendall anasema Putin amejitolea kuonyesh ubabe wake kupitia kuingilia kati Syria na Ukraine.

Aidha, Bw Putin anataka nchi za Magharibi zitambue haki ya Urusi ya kuchukulia nchi jirani zilizokuwa sehemu ya muungano uliosambaratika wa Usovieti kuwa maeneo yake na ambayo hayafai kuingia Nato au miungano mingine ya magharibi.