Kitabu kipya cha Game of Thrones kuchelewa

Game of Thrones Haki miliki ya picha AP
Image caption Kitabu cha Winds of Winter kilitarajiwa kuwa tayari mwaka huu ukianza

Mwandishi wa mwendelezo wa vitabu vinavyotumiwa katika filamu za Game of Thrones amesema kitabu kipya cha mwendelezo huo kitachelewa tena.

George RR Martin amesema bado hajamaliza kukiandika kitabu hicho kwa jina Winds of Winter.

Kitabu hicho kilitarajiwa kuchapishwa wakati mmoja ya kutolewa kwa filamu ya sita ya mwendelezo wa filamu za Game of Thrones mwezi Aprili.

Kundi la waandalizi wa filamu hizo kutoka HBO sasa wamefikia mwandishi huyo katika hadithi, baada ya kumaliza kutumia vitabu vya awali.

Filamu za Game of Thrones hutumia msururu wa vitabu vya George RR Martin vya A Song of Ice and Fire. Cha kwanza ndicho kilichoitwa A Game of Thrones na kilichapishwa mwaka 1996.

Akiandika kwenye blogu, George RR Martin amesema ameandika sehemu kubwa ya hadithi hiyo lakini kwamba bado atahitaji “miezi kadha…na hilo ni ikiwa kila kitu kitaenda sawa”.

“Niamini, haijanifurahisha kuandika haya. Mmesikitika, na hamko pekee.”

Kitabu cha tano cha Game of Thrones kwa jina A Dance with Dragons kilimchukua mwandishi huyo miaka mitano kukiandika kabla ya kuchapishwa kwake 2011.

Haki miliki ya picha hbo
Image caption Kitabu cha majuzi zaidi kiliitwa A Dance with Dragons

Mwandishi huyo amesema alitaka sana kumaliza kuandika kitabu hicho kabla ya kuingia mwaka 2016.

Amedokeza kwamba mashabiki hata hivyo hawafai kuwa na wasiwasi sana kwani makala ya sita ya mwendelezo wa filamu hizo utakuwa tofauti na hadithi ya kitabu.

Mwezi Julai mwaka jana HBO walisema kutakuwa na makala tatu zaidi za Game of Thrones, ukihesabu makala ya sita.