Gerrard apanga kurejea Liverpool

Steven Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Gerrrard alichezea Liverpool mechi 710

Nahodha wa zamani wa Liverpool Steven Gerrard anapanga kurejea katika klabu hiyo kama mkufunzi atakapoacha kucheza.

Mchezaji huyo wa miaka 35, aliyeshinda vikombe 10 akiwa na Liverpool, aliondoka mwisho wa msimu uliopita na kujiunga na Los Angeles Galaxy.

"Sina uhakika 100% lakini nafikiri labda huu mwaka utakuwa wangu wa mwisho kucheza,” Gerrard ameambia gazeti laDaily Telegraph.

"Nimezungumza na [meneja wa Liverpool Jurgen] Klopp. Klabu imenijulisha kwamba inataka sana nirudi."

Gerrard, alichezea Liverpool mechi 710 na timu ya taifa ya Uingereza mechi 114.

Anatarajia kuhitimisha uchezaji wake Novemba au Desemba mwaka huu.

Amekiri kwamba anajutia kutochukua mafunzo ya ukocha mapema, na kutoa wito kwa Shirikisho la Soka la England kuhakikisha wachezaji wanasalia katika kandanda baada ya kumalizika kwa kipindi chao cha uchezaji.

"Nasikitika kwamba sikuanza mafunzo ya ukocha nikiwa na miaka 21-22. Muda huo wote niliopoteza katika hoteli kama mchezaji wa England nikiwa na upweke nikitazama 'The Office' na 'The Sopranos',” alisema.

"Laiti ningekamilisha masomo ya ukocha, na sasa ningekuwa nimepata leseni.”