Watu wenye silaha wavamia kambi ya jeshi India

Pathankot Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Maafisa wa polisi wakilinda kambi hiyo baada ya shambulio

Washambuliaji wanne wameuawa baada ya wanajeshi wa India kuzima shambulio la mapema asubuhi katika kambi la jeshi la wanahewa karibu na mpaka wake na Pakistan.

Wanajeshi wawili wa kambi hiyo ya Pathankot pia waliuawa kwenye makabiliano na wapiganaji hao, ambayo yalidumu saa kadha.

Kambi hiyo imo kwenye barabara kuu ya kuelekea sehemu ya Kashmir inayodhibitiwa na Kashmir.

Shambulio hilo limetokea siku chache baada ya viongozi wa India na Pakistan Narendra Modi na Nawaz Sharif kukutana mjini Lahore kuzindua mpango wa ghafla wa kutafuta Amani.

Jimbo lote la Punjab nchini India limewekwa katika hali la tahadhari.

Watu hao walioshambulia kambi hiyo wanadaiwa kuvalia sare za jeshi la India na walitumia gari walilokuwa wameteka nyara.

Waliingia maeneo ya makazi ya wanajeshi kambini lakini wakakabiliwa vikali na hawakuweza kuharibu vifaa vya jeshi, msemaji wa jeshi la wanahewa Rochelle D'Silva amesema.

Mwandishi wa BBC Sanjoy Majumder akiwa Delhi anasema bado haijabainika washambuliaji hao walikuwa kina nani lakini wanashukiwa kutoka kundi la wapiganaji wa Kashmir kutoka upande unaodhibitiwa na Pakistan.

Hata hivyo, shirika la habari la AFP limemnukuu afisa mmoja wa usalama akisema wanaaminika kuwa wa kutoka kundi la Jaish-e-Mohammed.

India inamini kundi hilo husaidiwa na Pakistan, madai ambayo taifa hilo limekanusha.

Mwezi Agosti, watu saba waliuawa katika shambulio sawa, watu wenye silaha waliposhambulia kituo cha polisi wilaya ya Gurdaspur.