Al-Shabab wamtumia Trump wakitafuta wafuasi

Trump Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Trump alishutumiwa vikali kwa kupendekeza Waislamu wazuiwe kuingia Marekani

Kundi la wapiganaji wa Kiislamu la al-Shabab kutoka Somalia limetoa kanda ya video ya propaganda ambapo wanamtaja mgombea urais wa Marekani Donald Trump.

Hii imejiri wiki kadha baada ya Trump, anayeongoza kinyang’anyiro cha kutafuta atakayepeperusha bendera ya chama cha Republican, kupendekeza Waislamu wazuiwe kuingia Marekani.

Kundi la al-Shabab, ambalo lina uhusiano na mtandao wa Al-Qaeda, linaelekeza ujumbe kwa Wamarekani weusi, likiwahimiza kusilimu na kushiriki kwenye Jihad au vita vitakatifu.

Kundi hilo linasema kwenye video hiyo kwamba ubaguzi wa rangi, ukatili wa polisi na chuki dhidi ya Waislamu vimesheheni Marekani.

Wasimamizi wa kampeni ya Bw Trump hawajazungumza lolote kuhusu video hiyo.

Miaka ya hivi karibuni, Wasomali-Wamarekani kutoka Minnesota wameripotiwa kwenda Somalia kujiunga na al-Shabab.