Waisraeli washtakiwa kuua Wapalestina

Dawabsha Haki miliki ya picha EPA
Image caption Nyumba ya familia ya Dawabsha ilichomwa moto Julai mwaka jana

Maafisa wa mashtaka nchini Israel wamewashtaki washukiwa wawili kuhusiana na shambulio katika nyumba moja ya Wapalestina eneo la Ukingo Magharibi mwaka uliopita.

Watu watatu walifariki baada ya nyumba hiyo kuchomwa moto.

Amiram Ben-Oliel, 21, ameshtakiwa mauaji, huku kijana mwingine ambaye jina lake halijatolewa akishtakiwa kuwa mshirika katika mauaji.

Mauaji ya Saad na Riham Dawabsha na mtoto wao wa miezi 18 kwa jina Ali, katika kijiji cha Ali Julai mwaka jana yalishutumiwa vikali na jamii ya kimataifa.

Mtoto mwingine wa umri wa miaka minne, kwa jina Ahmed, bado anatibiwa majeraha ya moto.

Nyumba yao ilichomwa walipokuwa wamelala.

Kwa mujibu wa stakabadhi za mashtaka, Ben-Oliel alitekeleza shambulio hilo kulipiza kisasi mauaji ya mlowezi wa Kiyahudi mwezi mmoja awali.