Netanyahu atahadharisha Waisraeli Waarabu

Netanyahu Haki miliki ya picha Getty
Image caption Netanyahu amesema raia wote wa Israel lazima watii sheria

Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amesema usalama utaimarishwa zaidi katika maeneo ya Wairsaeli Waarabu baada ya mshambuliaji kuua watu wawili mjini Tel Aviv.

Akizungumza baada ya kutembelea eneo la shambulio Jumamosi, Bw Netanyahu alisema lazima watu wote watii sheria za taifa.

Polisi wanasema mshambuliaji alikuwa Mwisraeli Mwarabu mwenye umri wa miaka 29. Haijabainika lengo la mshambuliaji lilikuwa gani.

Watu saba pia walijeruhiwa wakati wa shambulio hilo la Ijumaa nje ya baa moja mashuhuri Tel Aviv, wanne kati yao vibaya.

Watu wawili wauawa na mshambuliaji Tel AvivBw Netanyahu aliwasifu viongozi wa Waisraeli Waarabu kwa kushutumu mauaji hayo, lakini akasema Israel inakabiliwa na hatari ya kuwa “taifa ambalo wengi wa raia wanaheshimu sheria, na taifa ndani ya taifa lenye uchochezi wa Kiislamu na silaha haramu ambazo mara kwa mara hutumiwa katika harusi, sherehe na visa vya uhalifu,” gazeti la Jerusalem Post limeripoti.

Alisema serikali yake inaimarisha juhudi za kuhakikisha utekelezaji wa sheria maeneo ya Negev, na Galilee, na eneo la Pembe Tatu, na kwingineko”.

Hili litashirikisha kujengwa kwa vituo vipya vya polisi na kuongezwa kwa maafisa wa polisi.

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Polisi bado wanamsaka mshukiwa

Mshukiwa wa shambulio hilo la Ijumaa anadaiwa kutoka kaskazini mwa Israel na alitumia bunduki aliyoiiba kutoka kwa babake kutekeleza mauaji hayo.

Babake alimtambua mwanawe kutokana na ripoti za vyombo vya habari na akawasiliana na polisi, gazeti la Haaretz linasema.

Shambulio hilo lilitokea baada ya kipindi cha msururu wa mashambulio ya Wapalestina dhidi ya Waisraeli ambayo yalikuwa yamesababisha vifo vya Waisraeli 21 kufikia 23 Desemba. Wapalestina zaidi ya 131 pia walikuwa wameuawa.