Trump azungumzia video ya al-Shabab

Trump Haki miliki ya picha AP
Image caption Trump ameendelea kusisitiza kwamba Waislamu wanafaa kuzuiwa kuingia Marekani

Mgombea wa urais Marekani Donald Trump kwa mara nyingine ametetea pendekezo lake la kutaka Waislamu wazuiwe kuingia Marekani baada ya wito huo kutumiwa na wapiganaji wa al-Shabab kwenye kanda ya video ya kutafuta wafuasi.

Bw Trump, anayeongoza miongoni mwa wanaotafuta tiketi ya chama cha Republican, amesema watu wamemsifu kwa kuwa na ujasiri wa kuangazia jambo hilo “ambalo wengine wameamua kupuuza”.

Al-Shabaab walitumia maneno hayo ya Trump kwenye video ya propaganda ya kutafuta wafuasi wakisema ubaguzi wa rangi, ukatili wa polisi na chuki dhidi ya Waislamu vimesheheni Marekani.

"Sasa watu wanaanza kuzungumzia hili,” ameambia kituo cha runinga cha CBS News.

Kundi hilo liliweka sehemu ya kanda ya video ya Trump akikariri wito wake wakati wa mkutano wa kampeni kwenye video yao ya propaganda ya karibu saa nzima.

Katika mahojiano na watangazaji wa kipindi cha Face the Nation cha CBS News, ambacho kitapeperushwa baadaye Jumapili, Bw Trump aliulizwa kuhusu jinsi al-Shabab wanatumia matamshi yake kutafuta wafuasi.

"Tazama, kuna shida hapa. Nimeibua hili. Watu wengine wamenipigia simu na kusema nina ujasiri kwamba niliibua hili kwa sababu ni ukweli mtupu na hakuna anayetaka kuhusika.

"Watu ambao wameshawishika vingine na sasa wanasema, unajua, labda Trump hajakosea. Tunafaa kuangalia hili kwa kina zaidi.”

Baadaye, Bw Trump alizungumzia video hiyo katika kanda hiyo ya Al-Shabab kwenye Twitter.

Bw Trump alipendekeza Waislamu wazuiwe kuingia Marekani baada ya wanandoa Waislamu kushambulia sherehe mjini San Bernardino, California na kuua watu 14.

Wito wake ulishutumiwa snaa na viongozi mbalimbali duniani.

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Matamshi ya Trump yalishutumiwa sana

Mgombea urais wa chama cha Democratic Hillary Clinton alisema maneno ya Bw Trump yanamfanya kuwa “mwandikishaji bora sana wa wanachama” wa kundi linalojiita Islamic State.

Miaka ya hivi karibuni, Wasomali-Wamarekani kutoka Minnesota wameripotiwa kwenda Somalia kujiunga na al-Shabab.

Wapiganaji wa al-Shabab, hutaka kuondoa madarakani serikali ya Somalia inayoungwa mkono na mataifa ya Magharibi na kuweka utawala mkali wa Sharia.

Wametekeleza mashambulio ya kigaidi Kenya, Uganda na Ethiopia.