Japan yataka mazungumzo ya amani na Urusi

Abe Haki miliki ya picha Getty
Image caption Abe na Putin walizungumzia visiwa hivyo mara ya mwisho 2013

Waziri Mkuu wa Japan Shinzo Abe ameitisha mazungumzo ya amani kati yake na Rais wa Urusi Vladimir Putin kujadili mkataba wa Amani kati ya nchi hizo mbili.

Mataifa hayo mawili hayakutia saini mkataba wa amani baada ya kumalizika kwa Vita Vikuu vya Pili vya Dunia kutokana na mzozo kuhusu umiliki wa visiwa vinne.

Bw Abe ameambia wanahabari kwamba viongozi wote wawili wanakubaliana kwamba ni jambo la kushangaza kuwa mkataba huo haujatiwa saini kwa miaka 70.

Tangu achukue uongozi 2012 Bw Abe amekuwa akijaribu kuimarisha uhusiano kati ya Tokyo na Moscow.

Muungano wa Usovieti uliteka visiwa kadha ambavyo Japan huviita Northern Territories mwaka 1945. Urusi huviita Southern Kurils.

Viongozi hao wawili walijadili suala hilo mara ya mwisho 2013.

Nchi hizo mbili zilirejesha uhusiano wa kidiplomasia mwaka 1956.

"Bila mkutano mkuu, tatizo la visiwa vya Northern Territories haliwezi likatatuliwa,'' alisema, alipokuwa akihutubia wanahabari kikao cha Mwaka Mpya.

Aliongeza kwamba ataendelea kuzungumza na Bw Putin “kila fursa inapotokea”.