Marekani yafunga kituo cha ndege Ethiopia

US Haki miliki ya picha AFP
Image caption Marekani imetumia ndege zisizo na rubani kuua viongozi kadha wa al-Shabab

Marekani imefungia kituo cha ndege zisizo na rubani nchini Ethiopia ambacho imekuwa ikitumia kushambulia wanamgambo wa al-Shabab katika taifa jirani la Somalia.

Maafisa wa Marekani wanasema kituo hicho cha siri kilikuwa cha muda tu na kwamba kwa sasa hakikihitajiki tena.

Kirasmi, Marekani ina kambi moja tu ya jeshi barani Afrika, ambayo imepewa jina Camp Lemonnier nchini Djibouti. Lakini huwa ina kambi nyingi za muda maeneo mengi barani.

Oktoba mwaka 2015, jarida la habari za ufichuzi The Intercept, lilichapisha nyaraka za siri za jeshi ambazo lilisema lilionyesha Marekani ilikuwa na kambi zaidi ya 14 za ndege zisizo na rubani barani Afrika.

Ndege hizo zimetumiwa kuua makamanda kadha wa al-Shabab, akiwemo kiongozi wa kundi hilo Ahmed Godane mwaka 2014.

Wakosoaji wanasema mashambulio hayo huwa hayapati shabaha wakati wote na mara nyingine huua watu wasio na hatia.

Vyombo vya habari Ethiopia vinasema Marekani ilianza kutumia kituo hicho kilichoko kusini mwa nchi hiyo 2011.

Ethiopia imekuwa mshirika wa karibu wa Marekani katika vita dhidi ya al-Shabab, na pia imekuwa na wanajeshi Somalia tangu 2006.