IMF yasema Nigeria haihitaji usaidizi

Nigeria Haki miliki ya picha AFP Getty
Image caption Nigeria imeathiriwa sana na kushuka kwa bei ya mafuta

Mkuu wa Shirika la Fedha Duniani (IMF) amesema Nigeria kwa sasa haihitaji usaidizi wowote wa kifedha licha ya uchumi wake kuathirika na kushuka kwa bei ya mafuta duniani.

Akiongea baada ya kukutana na Rais wa Nigeria Muhammadu Buhari mjini Abuja, Bi Christine Lagarde, amesema hata hivyo kwamba nchi hiyo inahitaji kupunguza utegemeaji sana wa mapato kutoka kwa mafuta.

Rais Buhari amesema moja ya malengo yake makuu ni kufufua uchumi wa taifa hilo lenye uchumi mkubwa zaidi barani Afrika.

Lakini anakabiliwa na changamoto kwa uchumi wa Nigeria umeathirika na kushuka kwa bei ya mafuta duniani.

Ukuaji wa uchumi wa Ngeria kwa sasa ni asilimia 3, kiwango cha chini zaidi katika kipindi cha miaka mingi.

Kiwango cha mfumko wa bei kimefikia 10 % na thamani ya sarafu ya Nigeria imeshuka.

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Nigeria ndiyo mzalishaji mkubwa wa mafuta Afrika

Serikali ya Nigeria, inayotegemea mapato kutoka kwa mauzo ya mafuta kufadhili nusu ya matumizi yake, pia imekumbwa na upungufu wa pesa.

Taifa hilo lilizindua bajeti kubwa zaidi katika historia yake mwaka jana, ikiwa ni mipango mingi ya miradi ya miundo mbinu.

Lakini wakosoaji wa serikali wanahofia hatua ya serikali kukopa pesa huenda ikaathiri uchumi.