Picha ya nguva iliyokataliwa na Facebook

Denmark Haki miliki ya picha Getty
Image caption Gjerskov aliambia mara ya kwanza kwamba picha hiyo ilikuwa inaonyesha utupu

Mwanasiasa mmoja nchini Denmark aliyejaribu kuweka picha ya sanamu ya nguva mtandaoni alishangaa baada ya kujulishwa na Facebook kwamba hangeruhusiwa kuipakia kwa sababu ilikuwa inaonyesha uchi.

Mbunge huyo wa chama cha Social Democrat, Mette Gjerskov alitaka kuchapisha kihusishi cha ukurasa wa blogu yake kikiwa na picha ya sanamu hiyo ya shaba, tovuti ya Ekstra Bladet imeripoti.

Sanamu hiyo ya nguva hupatikana mjini Copenhagen.

Ujumbe kutoka Facebook, ambao Gjerskov aliweka mtandaoni, unaonyesha alijulishwa kuwa picha yake hiyo ilikuwa “na uchi au maudhui ya kimapenzi”.

Alifahamishwa kwamba sera kuhusu kutochapisha picha za uchi hutumia pia hata kama picha ni ya mafunzo au ni kazi ya sanaa.

Gjerskov amesema uamuzi huo ni wa kushangaza sana.

Lakini anasema baadaye Facebook ililegeza msimamo na kukubali apakie picha hiyo.

Mwezi Machi 2015, Facebook ilifafanua sera yake kuhusu picha za uchi na kusema picha za michoro, sanamu na sanaa zinaashiria uchi zinakubalika.

Sanamu hiyo ya nguva si kazi ya kwanza ya sanaa nchini Denmark kuzuiwa kuchapishwa.

Mwezi Septemba, Kampuni ya Facebook ilizuia kampuni moja ya utalii kupakia picha ya mchoro wa mwanamke akiwa amesimama mbele ya kioo akiwa uchi, kabla ya kuikubali na kusema ilikuwa imezuiwa kimakosa.