Trump atumia wito kuhusu Waislamu tangazoni

Trump Haki miliki ya picha AP
Image caption Trump amesema atatumia karibu $2 milioni kwa matangazo ya televisheni kila wiki

Donald Trump ametumia wito wake wa kutaka Waislamu wazuiwe kuingia Marekani kwa muda kwenye tangazo lake la kwanza la kampeni kwenye televisheni.

Tangazo hilo lilipeperushwa runingani mara ya kwanza Jumatatu.

Aidha, anatumia pia wazo lake la kutaka ua ujengwe katika mpaka wa Marekani na Mexico kuzuia wahamiaji haramu kuingia Marekani.

Anataka ujenzi wa ukuta huo “ulipiwe na Mexico”.

Tangazo hilo la sekunde 30 linasimuliwa na sauti nzito ya kiume na linaonyesha pia picha za mgombea wa chama cha Democrat Hillary Clinton na Rais Barack Obama.

Aidha kuna picha za washambuliaji walioua watu 14 San Bernardino jimbo la California, wapiganaji wa Islamic State, manowari ya Marekani ikifyatua makombora, jumba likilipuliwa na wahamiaji wanaodaiwa kuwa wanavuka mpaka wa Marekani na Mexico.

Haki miliki ya picha Trump Campaign
Image caption Trump amependekeza ukuta ujengwe kuzuia wahamiaji kutoka Mexico kuingia Marekani

Tangazo hilo linamalizika kwa Trump kutoa kauli mbiu yake ya kutaka kurejesha tena fahari ya Marekani.

Bw Trump amesema atatumia karibu $2 milioni (£1.4 milioni) kila wiki kwa matangazo ya runinga katika majimbo ya Iowa na New Hampshire.