Mhubiri wa Kiislamu ahukumiwa kifo Nigeria

Haki miliki ya picha Getty
Image caption Mahakama za Kiislamu huwa hata na polisi wake Nigeria

Mahakama moja ya Kiislamu nchini Nigeria imemhukumu kifo mhubiri anayetuhumiwa kukufuru kwa kumtukana Nabii Muhammad.

Abdul Inyass amehukumiwa katika kikao cha faragha cha mahakama katika mji wa Kano, kaskazini mwa Nigeria.

Kikao hicho kimefanyika faraghani kuzuia “fujo kutoka kwa umma” sawa na ilivyoshuhudiwa wakati wa kikao cha awali, afisa wa mashtaka Lamido Abba Soron-Dinki ameambia shirika la AFP.

Bw Inyass alishutumiwa vikali Mei alipotoa matamshi ya kumtukana Nabii Muhammad kwa wafuasi wake, walipokuwa wakiadhimisha siku ya kuzaliwa kwa kiongozi wa zamani wa madhehebu ya Kisufi ya Tijaniyya, Ibrahim Niasse kutoka Senegal, shirika hilo linasema.

Bw Inyass anadaiwa kusema “Niasse alikuwa mkuu kushinda Nabii Muhammad”, matamshi yaliyozua maandamano mjini Kano.

Mhubiri huyo alikamatwa Agosti akiwa mafichoni mjini Abuja na akarejeshwa Kano kujibu mashtaka, Bw Soron-Dinki ameambia AFP.

"Ana muda wa mwezi mmoja kukata rufaa lakini wengi hawadhani atakata rufaa,” ameongeza.

Wafuasi watano wa Bw Nyass walihukumiwa kifo mwaka jana.

Madhehebu ya Tijaniya yalianzishwa na Ahmad Ibn Muhammad al-Tijani nchini Algeria mwaka 1784 na yana wafuasi wengi Afrika Kaskazini na Magharibi.

Maeneo ya kaskazini mwa Nigeria huwa na mfumo mbadala wa haki, ambapo mahakama za Kiislamu huruhusiwa kuhudumu.

Serikali ya kitaifa haijawahi kuruhusu mtu aliyehukumiwa kifo na mahakama za Kiislamu auawe.