Mshukiwa aliyejisalimisha Kenya rumande

Mohamed
Image caption Mohamed alijisalimisha kwa polisi Jumanne

Mshukiwa wa ugaidi aliyejisalimisha kwa maafisa wa usalama Kenya, amefikishwa mahakamani leo na kuwekwa rumande.

Mohamoud Salim Mohamed, ambaye ni mmoja wa washukiwa wanne wanaodaiwa kukwepa msako wa polisi mjini Mombasa Jumatatu, atazuiliwa kwa muda wa mwezi mmoja huku polisi wakichunguza uhusiano wake na kundi la al-Shabab.

Polise walimfikisha Bw Mohamed, ambaye pia hujulikana kama Gasere, mahakamani kisiri asubuhi.

Walimzuilia katika chumba kimoja mahakamani huku waandishi wa habari wakisubiri kwenye ukumbi rasmi. Baadaye aliwasilishwa kwa kupigwa picha tu.

Stakabadhi kutoka kwa polisi zinaonyesha kuwa anachunguzwa kwa tuhuma za kuwa mwanachama kwa kundi la kigaidi la al-Shabab.

Makachero pia wanaamini mshukiwa huyo ni mmoja wa wanNe waliokimbia operesheni kwenye nyumba moja mtaa wa Majengo, Mombasa ambapo silaha, vilipuzi na vyombo vya mawasiliano vilinaswa. Aidha Mohammed anadhaniwa kuvuka mpaka kutoka Somalia kwa wakati ambao bado haujafahamika.

Mohammed alijisalimisha kwa maafisa wa usalama mjini Malindi, kaskazini mwa Mombasa, akizindikizwa na babake Jumanne jioni.

Washukiwa hao wengine watatu wangali wanasakwa na polisi.

Hayo yakijiri, polisi nchini Kenya wameahidi zawadi ya jumla ya dola za Kimarekani 80,000 kwa habari zitakazosaidia kukamatwa kwa washukiwa wanne wanaodaiwa kuhusika katika shambulio la basi Mandera mwezi jana.