Manusura wa Boko Haram Nigeria

Watu zaidi ya 2 milioni wametoroka makwao nchini Nigeria, wakikimbia mashambulio ya wapiganaji wa Boko Haram katika kipindi cha miaka sita iliyopita.

Moja ya kambi kubwa zaidi za wakimbizi inapatikana katika eneo kame viungani mwa mji wa kaskazini mashariki wa Dalori, mahema ya rangi nyeupe yamepangwa mistari mirefu inayofikia zaidi ya kilomita.

Mwandishi wa BBC Jimeh Saleh alikutana na baadhi ya wakazi 18,000 wanaoishi katika kambi hiyo na kusikia simulizi zao kuhusu waliovyonusurika mashambulio ya wapiganaji hao wa Kiislamu na jinsi wanavyoendelea na maisha.

Mai Mutti

Mmoja wa watu wanaotambulika kwa urahisi kambi ya Dalori, Bw Mutti huchechemea na hutembea akitumia magongo.

Mfanyabiashara huyu wa zamani, mwenye umri wa miaka 55 kwa sasa, alitoroka mji wa Bama pamoja na maelfu wengine baada ya wapiganaji hao kuvamia mji huo 2014.

Alipigwa risasi mguuni, na ukaachwa ukining’inia.

"Nilikuwa nimelala walipofika alfajiri; Nilikuwa ninauguza jeraha la risasi ambalo nilikuwa nimepata shambulio lao la awali,” alisema.

Wapiganaji hao waliua mwana wao wa kiume wa umri wa miaka 24 na pia wakawateka nyara binti zake wawili.

Kwa sasa anaishi Dalori na wake zake wawili, watoto wengine 10 na wajukuu watatu.

Image caption Malaria na magonjwa ya kuharisha hutokea mara kwa mara kambini

Ukatili ambao yeye na majirani zake walipitia umefichwa na furaha iliyojiandika kwenye nyuso za watoto wao.

Watoto ndio wengi katika kambi hiyo na utawaona wakikimbia hapa na pale, wakiwa hawana kumbukumbu kuhusu mikasa ya awali na changamoto zinazowasubiri.

“Kesho utakuja tena, uje tena, uje tena,” wanaimba.

Lakini utapiamlo, malaria na magonjwa mengine vimeenea sana.

"Hili ndilo jambo mbaya zaidi nililowahi kushuhudia maishani,” anasema Noah Bwala, 60, ambaye ni afisa wa afya katika kambi hiyo.

Ma'aji Modu:

Huwezi kusikiliza tena

Mmoja wa wapishi wa jikoni kambi hiyo ni Bi Modu, ambaye bado hajui yaliyowasibu mumewe na watoto wao wanane.

Baadhi ya watoto wake walichukuliwa na wapiganaji hao kutoka mji wao wa Bama na wengine walitekwa nyara wakiwa shuleni.

"Huwa nalia sana kila nikiwakumbuka,” anasema.

Alipewa kazi ya kuwa mpishi baada ya kuhurumiwa na maafisa kambini. Walimhurumia kwa sababu hakuwa na familia.

Ya Ammuna

Huwezi kusikiliza tena

Miongoni mwa wazee kambini ni Bi Ammuna, anayesema ana umri wa miaka 100.

Mjane huyu ambaye zamani alikuwa akiuza maziwa bado ana uchungu kutokana na kupoteza nyumba zake mbili baada ya mji wa Bama kutekwa na Boko Haram.

Alipokonywa nyumba zake akiwa amenyooshewa bunduki na wapiganaji hao wa Kiislamu, anasema.

Lakini ana matumaini kwamba sasa, kwa sababu jeshi limefanikiwa kukomboa maeneo mengi ambayo awali yalikuwa yanadhibitiwa na Boko Haram, wanajeshi wataweza kumrejesha nyumbani itakapokuwa salama kurejea.

Bw and Bi Modu Bulama

Huwezi kusikiliza tena

Licha ya huzuni Dalori, baadhi ya wakazi bado hupata wakati wa kuchumbiana.

Modu Bulama mwenye umri wa miaka 35 aliingia kambini baada ya mkewe na watoto wawili kuuawa na Boko Haram.

Alipokuwa akisaidia kusambaza vyakula na vitu vingine vya misaada, alikuwa na mwanamke aliyekuwa amempoteza mumewe katika mashambulio ya Boko Haram.

Baada ya kuzungumza kwa muda, walielewana na kuoana.

Lakini kuwa kambini hakukuwazuia kutekeleza tamaduni, na alilazimika kulipa mahari ya $50 (£34) ili kumuoa mwanamke huyo, ambaye hakutaka jina lake litajwe.