Mwanamume auawa makumbusho ya Charlie Hebdo

Hollande Haki miliki ya picha APTN
Image caption Polisi hao wapya wataajiriwa kufikia 2017

Rais wa Ufaransa Francois Hallande ameahidi kuajiri polisi 5,000 zaidi katika juhudi za kuimarisha usalama Ufaransa huku taifa hilo likiadhimisha mwaka mmoja tangu kutokea kwa shambulio la Charlie Hebdo.

Muda mfupi baada yake kuzungumza, maafisa wa polisi walimpiga risasi na kumuua mshukiwa aliyejaribu kushambulia kituo cha polisi.

Awali, Rais Hollande alikuwa amewasihi polisi na walinda usalama wengine kushirikiana katika kufanya ujasusi.

Hollande amesema polisi hao wa ziada wataongezwa kufikia 2017. Kadhalika, nafasi 2,000 zitaongezwa katika idara ya ujasusi.

Punde baada ya hotuba yake katika makao makuu ya polisi Ufaransa, habari zilitokea kuhusu kisa hicho kilichotokea mtaa wa 18, kaskazini mwa Paris.

Kulingana na maafisa wa usalama, mshukiwa huyo alisema ‘Allahu Akbar’ (Mungu ni Mkubwa) nje ya kituo cha polisi eneo la Goutte d’Or karibu na Montmartre, kabla ya polisi kumpiga risasi.

Ripoti zinasema mshukiwa alikuwa na kisu na mkanda wa kujiua.

Roboti ya polisi inayotumika katika machunguza na kutegua mabomu inatumiwa kuchunguza mwili.

Mwaka mmoja uliopita polisi waliwauwa wapinganaji watatu wa Kiislamu waliokuwa wameshambulia watu siku tatu Paris. Lakini bado kuna shaka kuhusu iwapo washambuliaji hao walikuwa na washirika Mashariki ya Kati.

Polisi watatu walikuwa miongoni mwa watu 17 waliouawa wapiganaji hao waliposhambulia afisi za gazeti la Charlie Hebdo na duka la jumla la Wayahudi kati ya 7-9 Januari mwaka jana.