Netflix yazua msisimko barani Afrika

Hastings Haki miliki ya picha Getty
Image caption Reed Hastings alitangaza kupanuliwa kwa huduma za Netflix Jumanne mjini Las Vegas

Kampuni ya Netflix, inayotoa huduma za video mtandaoni moja kwa moja, imezinduliwa katika mataifa karibu yote duniani na kuzua msisimko mkubwa.

Kunao wanaoamini itatoa ushindani kwa zinazotoa huduma za runinga, filamu na video kwa malipo.

Wengi wanaitazama kama njia ya kuwawezesha kupata video, ambazo awali walikuwa hawawezi kuzipokea, kwa urahisi na kwa bei nafuu.

Lakini wapo wanaopokea habari hizo kwa shaka kidogo, wakisema gharama ya kutumia huduma za mtandao pamoja na kasi yake, vitaifanya vigumu kwa wengi kunufaika.

Kampuni ya Netflix ilitangaza Jumanne kwamba itapeleka huduma katika nchi 130 zaidi.

Mataifa pekee ambayo haijafanikiwa kufika ni Uchina, Korea Kaskazini, Syria na Crimea.

Afisa mkuu mtendaji wa kampuni hiyo Reed Hastings ametangaza upanuzi huo katika maonyesho ya teknolojia ya CES yanayoendelea mjini Las Vegas nchini Marekani.

Amethibitisha pia kwamba Netflix itaanza kutoa video za HDR baadaye mwaka huu.

Haki miliki ya picha Getty
Image caption Orange is The New Black ni moja ya vipindi vinavyotayarishwa na Netflix

Hisa za kampuni hiyo zilipanda sokoni 9% baada ya tangazo hilo kutolewa.