Tanzania kutimua wageni wasio na vibali

Masauni Haki miliki ya picha Statehouse Tanzania
Image caption Bw Hamad Masauni alipokuwa akiapishwa

Tanzania imeanza rasmi operesheni ya kuwasaka na kuwafurusha raia wa kigeni wanaoishi na kufanya kazi nchini humo kinyume cha sheria.

Naibu waziri wa mambo ya ndani wa Tanzania Hamad Masauni ameambia wanahabari kwamba operesheni hiyo imeanzishwa baada ya kubainika kwamba kuna raia wengi wa kigeni wanaofanya kazi Tanzania kinyume cha sheria.

Operesheni hiyo hiyo inafanyika siku chache baada ya wizara inayohusika na ajira kumuagiza kamishna wa kazi nchini humo kufuta vibali vya kazi vya muda kwa wageni.

"Serikali haiwezi kukaa kimya wakati vijana wanakosa ajira huku kazi zile walizotakiwa kufanya zikifanywa na raia wa kigeni,” Bw Masauni amenukuliwa na gazeti la Mwananchi.

Afisa wa uhamiaji wa mkoa wa Dar es Salaam John Msumile amesema wanatarajia kuwakamata wageni zaidi ya 350.

Kuhusu vibali va kazi vya muda, Bw Masauni amesema serikali itaandaa utaratibu mwingine wa kushughulikia watu wanaotaka kufanya kazi Tanzania kwa muda.

Hii ni baada ya serikali kupokea malalamiko mengi kuhusu suala hilo.

Mwishoni mwa mwaka waziri katika afisi ya waziri mkuu anayehusika na ajira Jenista Mhagama pamoja na naibu waziri Anthony Mavunde walifanya ziara za kushtukiza katika kampuni mbalimbali.

Waligundua raia kadha wa kigeni waliokuwa wakifanya kazi bila vibali halali.