Maafisa wa usalama Ethiopia 'waua watu 140'

Ethiopia Haki miliki ya picha AFP
Image caption Serikali imesema watu watano waliuawa katika maandamano mwezi uliopita

Maafisa wa usalama Ethiopia wamewaua watu zaidi ya 140 walioshiriki maandamano ya kupinga serikali tangu Novemba, wanaharakati wanasema, kwa mujibu wa shirika la Human Rights Watch (HRW)

Maandamano hayo yanatokana na wasiwasi kwamba mpango wa kupanua mji mkuu wa Addis Ababa na kuingia maeneo ya Oromia utawapokonya mashamba wakulima wa Oromo.

Maafisa wa HRW pia wametoa wito kwa serikali kumwachilia huru mwanasisa wa jamii ya Oromo aliyekamatwa mwezi uliopita.

Serikali imedai watu wanaoandamana wana uhusiano na makundi ya kigaidi.

Mwezi uliopita, maafisa wa serikali walisema watu watano waliuawa wakati wa makabiliano kati ya waandamanaji na maafisa wa usalama.

Maafisa kadha wa usalama, ambao idadi yao haikutajwa, pia walifariki.

Kwa mujibu wa sensa ya 2007, Waoromo ndio kabila lenye watu wengi zaidi Ethiopia, likiwa na watu 25 milioni kati ya raia wote 74 milioni nchini humo.