Mwanachama wa IS amuua mamake hadharani

IS Haki miliki ya picha AP
Image caption Kundi la IS hutekeleza sheria kali za Kiislamu

Mpiganaji wa kundi la Islamic State nchini Syria amemuua mamake hadharani kwa sababu alimwambia ahame kundi hilo, wanaharakati wanasema.

Ali Saqr, 21, alimuua mamake, Lena al-Qasem, 45, nje ya afisi ya posta mjini Raqqa, Syria, watu walioshuhudia wanasema.

Mji wa Raqqa umekuwa ukihudumu kama mji mkuu wa IS tangu wapiganaji hao kutekwa mji huo Agosti 2013.

Kundi hilo huwa halivumilii watu wanaopinga msimamo wake na kutoa adhabu kali kwa wanaopinga kundi hilo, na mara nyingi adhabu hutekelezwa hadharani.

Maafisa wa Shirika la Syrian Observatory for Human Rights (SOHR) lenye makao yake Uingereza na kundi la wanaharakati wa Raqqa is Being Slaughtered Silently (Raqqa Inachinjwa Kimy akimya) wamethibitisha kisa hicho.

Lena al-Qasem alikuwa amemwambia mwanawe kwamba muungano unaoongozwa na Marekani ungeangamiza kundi hilo, na akajaribu kumshawishi ahame mji huo pamoja naye.

Mwanawe alijulisha wenzake katika IS, na agizo likatolewa auawe.

Ali Saqr anadaiwa kumpiga risasi mamake nye ya afisi ya posta mbele ya mamia ya watu.

Kundi la IS hutekeleza sheria kali za Kiislamu, zenye kuegemea madhehebu ya Kisuni.

Kundi hilo limedhibiti maeneo ya Iraq na Syria tangu 2014.