Wafungwa 50 watoroka jela DR Congo

Wafungwa wapatao 50, wakiwemo watu waliohukumiwa mauaji, wametoroka kutoka gereza moja nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, afisa wa serikali ameambia shirika la AFP.

Wafungwa hao walitumia fursa ya kuzuka kwa moto katika gereza lililoko mji wa Kamituga kutoroka.

Mji huo hupatikana kilomita 170 kusini magharibi mwa mji wa Bukavu, mji mkuu wa mkoa wa Kivu Kusini.

Waliotoroka ni pamoja na "wanaume 20, wawili waliohukumiwa kwa mauaji na 18 kwa ubakaji,” Desire Kubuya Masumbuko ameambia shirika la habari la AFP.

Hakuna mfungwa hata mmoja aliyenaswa tena.

Wanahabari wanasema visa vya wafungwa kutoroka jela DR Congo, ambako magereza huwa yamejaa wafungwa kupita kiasi na hali huwa mbaya, hutokea mara kwa mara.

Maeneo ya Mashariki mwa DR Congo yameathiriwa kutokana na mapigano kuhusu udhibiti wa ardhi na madini, ambayo yameendelea kwa zaidi ya miaka 20.