Uchaguzi wa urais CAR waingia duru ya pili

Dologuele Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Dologuele, aliyeongoza, alipata asilimia 24 ya kura zilizopigwa

Mawaziri wakuu wawili wa zamani nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati watakutana katika duru ya pili ya uchaguzi nchini humo baada ya kukosekana kwa mshindi wa moja kwa moja wakati wa duru ya kwanza.

Mshindi hutakiwa kupata asilimia 50 ya kura zilizopigwa.

Anicet Georges Dologuele, aliyeongoza alipata 24%, na atakutana na Faustin Touadera, aliyepata 19% ya kura, kwenye duru ya pili tarehe 7 Februari.

Bw Dologuele alikuwa waziri mkuu kati ya 1999 na 2001, na pia alihudumu kama waziri wa fedha nchini humo.

Bw Touadera alikuwa waziri mkuu katika serikali ya rais Francois Bozize, aliyepinduliwa 2013.

Watu zaidi ya milioni moja walishiriki uchaguzi huo mkuu wiki iliyopita, ambao ni wa kwanza tangu mapinduzi ya serikali ya Machi 2013.

Taifa hilo limegawanyika kwa misingi ya kidini.

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Touadera alikuwa amechukua uongozi wa mapema

Wagombea 20 kati ya 30 waliotaka kumrithi kaimu rais Catherine Samba-Panza walikuwa mapema wiki hii wamelalamikia udanganyifu uchaguzini na kutaka kura ziache kuhesabiwa na uchaguzi urudiwe.

Lakini wengi wao walishawishiwa baadaye na serikali ya mpito kuondoa malalamiko yao, na mahakama ya kikatiba inatarajiwa kuchunguza madai yao.

  • Anicet Georges Dologuele 23.8% - 281,420
  • Faustin Touadera 19.4% - 229,564
  • Desire Kolingba 12.6% - 149,134
  • Martin Ziguele - 10.8% - 121,009

Kura 1,181,115 zilipigwa, wapiga kura waliojitokeza wakiwa 79%

Chanzo:Tume ya uchaguzi CAR