Mwigizaji wa Hollywood alikutana na El Chapo

Haki miliki ya picha RollingStone
Image caption Sean Penn na El Chapo

Maafisa wa serikali nchini Mexico wamesema walijiandaa kumkamata kinara wa uuzaji wa madawa ya kulevya Joaquin Guzman maarufu kama El Chapo baada ya kufanya mahojiano na mwigizaji wa Hollywood Sean Penn.

Inasemekana serikali ilikuwa ikifuatilia nyendo za bwana Penn baada ya kukutana kwa siri na kinara huyo wa madawa ya kulevya katika eneo lililojificha mwezi October mwaka jana.

Katika mahojiano na jarida la Rolling Stone, El Chapo Guzman alisema yeye ndiye baba wa biashara ya madawa ya kulevya duniani ambapo anasafirisha kwa ndege na meli za chini kwa chini mwa bahari.

Bwana Penn alisema alifanya mahojiano hayo kwa sababu Wamerekani ni sehemu ya watumiaji wakubwa wa madawa hayo yenye athari na vurugu za mauaji.

Wakati huo huo Mexico imesema inajiandaa kumsafirisha El Chapo Guzman nchini Marekani ili kwenda kuyakabili mashitaka yake lakini wanasheria wake wanasema watapambana kuzuia suala hilo.