Rwanda yasema iko tayari kwa CHAN

Chan
Image caption Michuano ya CHAN itaanza Jumamosi tarehe 16 Januari

Rwanda imesema imejiandaa vya kutosha kwa mashindano ya kuwania kombe la taifa bingwa Afrika kwa wachezaji wa ligi za nyumbani, maarufu kama CHAN.

Katika mazungumzo na waandishi wa habari waziri wa michezo Uwacu Julienne amesema kwamba serikali imeondoa malipo ya visa kwa Waafrika wote watakaotaka kuhudhuria mechi za CHAN.

Amesema: "Kila kitu kiko tayari …viwanja, mahoteli, usalama na mahitaji yote ya kuandaa mashindano ya kiwango hiki."

Ameongeza kuwa miundombinu pekee yaani ujenzi na ukarabati wa viwanja vitakavyotumiwa, iliigharimu serikali milioni 18 dola za Marekani.

Mashindano ya CHAN yataanza kutifua vumbi tarehe 16 mwezi huu.

Mechi ya ufunguzi ni kati ya wenyeji Rwanda na Ivory Coast kwenye uwanja wa taifa Amahoro.

Viwanja vingine vitakavyotumiwa ni uwanja wa Nyamirambo mjini Kigali, uwanja wa Huye Kusini mwa nchi na uwanja wa Umuganda mjini Rubavu karibu na mpaka wa Jamuhuri ya kidemokrasia ya Congo.