Wanaharakati wamtafuta Rwomushana

Image caption Charles Rwomushana

Wanaharakati wa haki za binadamu na marafiri wa jasusi wa zamani nchini Uganda Charles Rwomushana wanasema kuwa hawajui aliko tangu akamatwe na polisi siku ya Ijumaa.

Wanaharakati wanasema kuwa walienda kwenye makao makuu ya ujasusi katika mji mkuu Kampala siku ya Jumamosi lakini wakaambiwa kuwa hakuwa akizuiliwa huko.

Msemaji wa wizara ya masuala ya ndani nchini Uganda, anasema kwa bwana Rwomushana alikuwa chini ya kuzuizi cha polisi na kukana madai kuwa amenyimwa fursa ya kukutana na mawakili wake.

Bwana Rwomushana alikamatwa baada ya kuchapisha picha kwa mtandao wa Facebook ambayo ilidaiwa kuonyesha maiti ya mkuu wa ulinzi wa mgombea wa upinzani Amama Mbabazi, Christopher Aine.

Upande wa bwana Mbabazi unawalaumu polisi kwa kumteka nyara bwana Aine mwezi uliopita. Utawala unakana ukisema kuwa amekimbia kwa sababu anatafutwa kwa kuongoza mashambulizi dhidi ya wafuasi wa rais Yoweri Museveni.