Picha za Salah Abdeslam zaibuka

Image caption Picha hizi zilinaswa na camera za CCTV katika kituo kimoja cha mafuta nchini Ufarasa siku moja baada ya mashambulizi ya Paris

Picha za kwanza za mshukiwa wa shambulizi la mji wa Paris Salah Abdeslam zimeripotiwa kuibuka, kwa mujibu wa kituo cha runinga cha urafansa BFM.

Picha hizo zilinaswa asubuhi ya tarehe 14 mwezi Novemba na camera za CCTV katika kituo kimoja cha mafuta nchini Ufarasa siku moja baada ya mashambulizi yaliyosababisha vifo vya watu 130.

Katika picha hizo Salah Abdeslam anaonekana mtulivu akitembea huku akiwa ameweka mikono yake mfukoni.

Salah Abdeslam anaripotiwa kuwaita marafiki zake wawili Mohammed Amri na Salah Hamza Attou akiwa mjini Paris mapema tarehe 14 mwezi Novemda waje kumpeleka nchini Ubelgiji.

Image caption Salah Abdeslam bado hajapatikana.

Wakiwa njiani kutoka Paris kwenda Brussels, wanaume hao watatu walisimama katika kituo cha mafuta karibu na mpaka wa Ubelgiji kwa takriban dakika 15 ambapo Camera ya CCTV iliwanasa.

Wakati huo wanaume hao tayari walikuwa wamepita katika vizuizi vitatu vya polisi, lakini hawakusimamishwa kwa sababu Salah Abdeslam hakuwa amehusishwa na mashambulizi ya Paris.

Mohammed Amri na Salah Hamza Attou baadaye waliamuacha Salah Abdeslam katika wilaya ya Laeken mjini Brussels, na wawili hao walikamatwa katika eneo la Molenbeek siku moja baadaye na sasa wanakabiliwa na mashtaka ya ugaidi huku Salah Abdeslam akiwa bado hajapatikana.